MTOTO wa miaka miwili badala ya kusema kikombe akatoa tusi, hufai kumpiga wala kumgombeza.
Unachotakiwa kufanya ni kumtia nguvu katika juhudi zake za kujifunza na
kumwambia kwa usahihi neno kikombe linavyotamkwa. Hivyo ndivyo hata kwa
mtu mgeni katika miji mikubwa.
Mshamba akitoa huko mashambani na kukutana na lifti katika majengo
makubwa na kutaka kuvua viatu kisha ndio aingie, ukimcheka utakuwa juha.
Sasa unamcheka nini na hayo mambo kwao hakuna? Unashanga kitu gani yeye
kuvua viatu na kutaka kuingia katika lifti wakati huko kwao kafundishwa
ni ustaarabu ukikuta maeneo nadhifu uvue viatu?
Nimetoa mifano hiyo nikikumbuka tabia ya msanii Baraka Da Prince. Kwa
siku za hivi karibuni bwana mdogo amekuwa na matukio na kauli za ajabu
na cha kushangaza watu wanamshangaa na wengine kumtolea maneno makali.
Ni kweli Baraka anafanya mambo ya kijinga, yasiyofaa kufanywa na mtu
anayejitambua. Ila mimi sishangai hayo mambo kufanywa na mtu aina ya
Baraka.
Yangefanywa na Diamond, Ali Kiba na akina Chegge ningeshangaa mno.
Nishangae vipi Baraka kuposti nyumba ya mama yake Naj na kusema ni yake
wakati najua kijana wetu huyu bado hajatokwa matongotongo machoni?
Katu siwezi kushangaa na yeyote atakayemshangaa, nitamshangaa yeye. Ni
jambo linalotarajiwa kabisa kwa kijana ambaye miaka mitatu nyuma alikuwa
akishindia kababu na mihogo huku akiwa ndani ya kaptura chafu
isiyojulikana rangi yake, viatu vilivyotoboka na akiwa anadhihakiwa na
kila msichana anayejaribu kumchombeza, kuwafanyia unyama ndugu zake kisa
kuwa na msanii Naj katika mapenzi.
Baraka ni kwanini asitokwe na akili kwa Naj wakati miaka mitatu
iliyopita alikuwa akimuona bibie katika magazeti na majarida akiwa
kakumbatiwa na Mr Blue, msanii ambaye Baraka huyu amekuwa akimuona toka
kipindi anaomba Shilingi ishirini akanunue ice cream kwa mama John?
Siwezi kumlaumu Baraka. Kumlaumu Baraka kwa ujinga anaoufanya ni sawa na
kulaumu mtoto mdogo anapotukana kipindi akijifunza kuongea.
Siku moja katika mitandao ya kijamii Baraka baada ya kuposti picha ya
mpenzi wake, Najma Dustan, msanii mwenzake, mtoto wa mjini Msami
akamtania kwa kujifanya anamtamani Naj.
Kilichotokea kiliniacha hoi kwa kicheko. Baraka akatokwa na matusi kwa Msami na kumwambia akamtamani dada yake.
Baraka anatupa maneno haya kwa mtu ambaye amekuwa akionekana katika video na magazeti kwa zaidi ya miaka sita sasa.
Anatokwa povu la kijinga kwa Msami kwa kudhani kuwa eti ni kweli
anamtamani mpenzi wake huku akiwa amesahau ni Msami huyu ambaye aliwahi
kudaiwa kutoka na mastaa wengine wakubwa wa Bongo.
Msami ni mtoto wa mjini sana kuliko Baraka. Msami kaona mengi ya
kimjini kuliko yeye. Kutoka dansa hadi kuwa msanii mwenye kueleweka,
Baraka anatakiwa ajue uzito wa Msami.
Yeye bado ni mgeni katika jumba la mastaa, anayofanya ni sehemu ya
ulimbukeni wa kawaida kwa mgeni. Kumlaumu au kumkosoa sana ni kumkosea.
Anayofanya Baraka ni sawa na mtu ambaye hajawahi kumiliki au kuendesha
gari zuri la thamani. Atatembea kila eneo kutaka kuonesha kuwa
anaendesha gari zuri. Huu ni ulimbukeni.
Muda ukipita atakomaa.
No comments:
Post a Comment